Saturday, September 4, 2010

MAPINDUZI YA BINTI WA LEO

Hiki ni kizazi kinachopitia mambo mengi katika ulimwengu huu wa sasa. Misukosuko katika kila kona ya maisha ni kama wamesahaulika na hawana msaada kabisa, hawana Imani na mtu yeyote wamekosa tumaini. Wengine hata wameanza kuzeeka kabla hata ya muda wao kwa sababu ya mizigo mizito waliyobeba uchungu, hofu, mawazo wanaona kama dunia yote ni giza, wameshapatwa na misukosuko mingi kuliko hata sisi wazazi wao tulioishi miaka mingi zaidi yao. Je sisi wazazi tunasemaje kuhusu mabinti zetu? tunakaa na kuongea nao kweli au ndio tunawarushia maneno mabaya kila siku? Tujue kuwa sisi wazazi ndio tunaowapa watoto wetu baraka au laana. Je ulishawahi kama mzazi kumbariki mwanao? au binti yako akishavunja ungo tu basi mnaanza mashindano na kuanza kuwawazia mawazo (mambo) mabaya. Ulishachukua muda ukaongea naye ukajua kuwa ni yapi yanayomsibu awapo nyumbani wakati wewe haupo, awapo shuleni, awapo njiani kwenda sehemu yeyote? Umewahi kujua Binti yako anawaza nini katika akili yake. Umewahi kumpa nafasi ya kusema jambo ukalisikiliza na kulipa kipaumbele. Maana jamani dunia ya leo si kama ya miaka ile sisi wengine tulivyolelewa, ambapo binti / kijana/ mtoto analelewa na Bibi na Babu, Shangazi na Mjomba, Jirani na hata mpita njia tu. Dunia ya sasa watoto wanajilea wenyewe na sisi wazazi wao tupo. Wanadamu tumekuwa wabaya kuliko hata simba jike mwenye watoto na halafu ana njaa. Hakuna baba, wala mama, wala kijana, si mjomba si shangazi kila mtu amekuwa simba jike. Je umeshafikiria mtoto wako anaishije? vikwazo gani anavyokumbana navyo. Tuamke jamani wazazi wenzangu kwa akili zetu wenyewe hatuwezi,  kwa mali tulizonazo bado na fedha bado si cho chote hatuwezi kulea watoto wetu vyema katika ulimwengu huu wa sasa tunahitaji msaada wa mwenye uweza na nguvu kutushinda sisi wanadamu na ni Mungu pekee ndio jibu na kimbilio letu ambaye anao uweza wa kutuwezesha kuwalinda na kuwalea watoto wetu.
TUBADILIKE WAZAZI WENZANGU.
Binti usivunjike moyo bado tumaini lipo bado nafasi unayo kwa yote uliyopitia bado liko penzi la kweli bado unaweza kuanza mwanzo mpya wenye mafanikio. Haijalishi wewe ni mfanyakazi wa ndani , haijalishi wewe ni yatima, haijalishi wewe umekimbia nyumbani nasema tena tumaini bado lipo. UNAHITAJI MAOMBI EWE BINTI EWE MZAZI, USHAURI n.k karibu sana nipo tayari kukuombea usiwe na wasiwasi kwa muda wote masaa 24 tuma maombi yako kwenye e-mail yangu nipo na wamama wengine waliojaa nguvu watakuombea pia.
USIKATE TAMAA BADO TUMAINI LIPO KARIBU SANA NA MUNGU WANGU AZIDI KUKUTIA MOYO NA KUKUBARIKI.