Tuesday, November 30, 2010

IMANI YAKO ITAKUPONYA, MWAMINI BWANA YESU LEO

Kila mwaka tarehe 1 / 12 ni siku ya kuadhimisha janga la UKIMWI kwa kuwa na ujumbe mbalimbali jinsi ya kutokomeza na kuelemisha watu jinsi ya kujikinga na kuzuia maambukizo mapya ya virusi vya UKIMWI na vile vile kuishi kwa matumaini kuhusiana na ugonjwa huu. Japo kuna baadhi ya maeneo elimu bado sijui niseme ni changa au haijawafikia walengwa vizuri, na  la kushangaza yakiwemo baadhi ya maeneo ya mijini yakiongoza kwa asilimia kubwa ya kuwa na maongezeko mapya ya mambukizi ya virusi vya UKIMWI. Swali la kujiuliza ni kuwa watu hawataki kuelewa au ni elimu imezoeleka kiasi kwamba watu wanaona hakuna jipya au maisha ndio yanawalazimisha kutokuzingatia yanayosemwa. Au je waelemishaji nao pia hawana elimu ya kutosha ya kuwaelimisha watu / watoaji elimu ni wachache kuliko walengwa / walioathirika? au wamekosa imani na Asasi / NGO zinazotoa huduma hii? Ukiangalia kwa mtazamo wa kawaida tu kuna Asasi/NGO mbalimbali zimeazishwa kwa ajili ya kusaidia na kuelimisha waathirika wa UKIMWI / na ambao bado hawajapata maambukizi pamoja na watoto yatima na wajane. Je wanatoa elimu sahihi na yakutosha? kama ndio kwa nini kuna ongezeko kubwa la watoto yatima na maabukizi mapya yanaibuka siku hadi siku? au waanzilishi  wa hizi Asasi / NGO wanatafuta maslahi yao wenyewe kwa kupitia mgongo wa walioathirika badala ya kutoa elimu ya sahihi na ya kutosha? Japo kwenye takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania imeshuka kwenye kiwango cha maambukizi ya UKIMWI ukilinganisha na nchi nyingine za Africa. Je hili nalo ni kweli yanaweza kuwa ongezeko la maambukizi mapya limepungua wakati bado tunashuhudia watoto yatima wakiongezeka kutokana na hili janga? (Tutafakari hili) Mimi sina jibu ila haya yote ni mtazamo wa kibinadamu tu. Hebu tungalie Biblia inatuambia nini kwa habari ya magonjwa? Je kuna ambalo linashindikana kwa Bwana? Kama yeye alitufinyanga kwa mikono yake si anajua kila sehemu ya viungo vyetu hivyo ni rahisi yeye kuturekebisha pale penye madhaifu na kupatia uzima. Hebu tuone Biblia inasema nini basi kwa habari ya uponyaji....

Ukisoma kwenye Biblia zetu utaona kwamba UKOMA ndio uliokuwa ugonjwa mbaya sana na ulikuwa unatishia watu enzi hizo za kale pia ulikuwa ni ugonjwa usioponyeka lakini watumishi wa Mungu walikuwa wanauwezo wa kuwaponya watu kutokana na ugonjwa huu kilichokuwa kinahitajika ni Imani na kutii tu, kwa Mfano Naaman aliyekuwa unaukoma lakini alipokea uponyaji. Soma 2Wafalme 5: 8-19 na pia Soma Mathayo 8:1-4 Yesu anaponya ukoma.

Japo kwa jambo la kushangaza na la kuhuzunisha ni kuwa huu ugonjwa hadi sasa upo toka enzi za akina Musa hadi leo lakini je ni kwamba dawa za kuuponya huu ugonjwa haijapatikana? imepatikana na ipo sema watu hawatilii maanani. Wako wapakwa mafuta wa Bwana ambao wamepewa karama ya kuponya wanaponyesha huu ugonjwa, kadhalika na UKIWMI pia wako watumishi wapakwa mafuta wa Bwana waliopewe karama ya uponyaji wako kukusaidia leo. Kama huu UKOMA ambao ulikuepo toka enzi hizo za akina Musa unawezekana kuponyeka kwanini watu wasiamini kuwa hata UKIMWI waweza kupona? Ukimwamini Mungu na kuyashika maagizo yake na kutii hakika utapona.

Mfano wa mwanamke aliyetoka damu kwa miaka kumi na miwili biblia inatuambia kuwa yule mwanamke aliazimia kuwa akiweza kushika tu upindo wa vazi aliyovaa Yesu hakika atapona na kweli alivyofanya hivyo kwa Imani yake kuu aliyokuwa nayo alipokea uponyaji muda ule ule Soma Mathayo 9 : 20 - 22; pia kwenye Marko 5: 25-34; sasa je wewe wawezaje kukata tamaa na kushindwa kumwammini Yesu kuwa kwa jina lake tu magonjwa yanatoweka hayatakuwa na nafasi tena ndani ya maisha yako utapona na utakuwa na nguvu na mwenye afya tele.  

Kama bado haujaambukizwa acha njia zako mbaya mtafute YESU shika maagizo yake na kuyatenda hakika atakuponya na hili janga wewe na familia yako na watu wa nyumbani mwako. Ingawa unaweza kuwa mwaminifu, waweza kuwa unatenda yaliyo mema kwa mtazamo wa kibinadamu lakini bado ukaupata huu ugonjwa kwa njia nyingine kwa mfano katika ajali kama ya gari, pikipiki au njia yoyote ile nk. (unajua kuwa maambukizi waweza pata kwa njia nyingi si kwa kuzini tu japo kuzini ndio njia kubwa ya maambukizi haya ya virusi vya UKIMWI). Lakini ukimtegemea Mungu na kukubali kuwa Yesu alikufa msalabani kwa ajili yako  na kuyatenda yote aliyokuamuru, hali hii haitakupata wewe na familia yako kwa ujumla na hata hutaacha wanao yatima bali utaishi hadi miaka mia na ishirini na utakufa ungali ukiwa na nguvu zako.

Yesu alifanya miujiza mingi ya uponyaji na hata sasa bado anafanya kwani anawatumia watumishi mbalimbali kufanya kazi aliyoianzisha kinachoturudisha nyuma ni kutokutilia maanani na imani kuwa haba kama nilivosema hapo juu. Watu tumekuwa na kiburi tukidhani kuwa wanayofanya watumishi wa Mungu ni ya uongo lakini mimi nakusihi leo hebu mwamini Yesu halafu utaona matunda yake na hakika hautajuta. Soma mistarii hii ikusaidie kwa habari ya imani katika uponyaji Mathayo 8 : 5-13; Mathayo 8 : 14-17;
Mathayo 9 : 27 - 31 n.k.

Mwamini yeye leo mtumainie Bwana peleka haja zako kwake naye atatenda, atakushindia na pia atakuponya, usikate tamaa usihangaike ikuze imani yako kwa kusikiliza na kusoma neno la Mungu mara kwa mara kwani Biblia inasema hivi "Imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa Neno la Kristo"
Warumi 10 : 17 kisha mweleze shida yako peleka haja zako kwake naye atafanya. Pia Yesu anasema hivi, hata ukiwa na Imani kiasi cha punje ya haradali ukisema mlima huu ung'oke mahali hapa uende kule, nao utang'oka. Hivyo basi na uponyaji wako unahitaji imani yako kidogo tu kama punje ya haradali kwa Yesu kuwa anaweza kukuponya nawe utapokea uponyaji. Tumwamini yeye tuuone mkono wa Bwana ukitenda ndani ya maisha yetu.

Sasa basi watoto waliojaa matumaini wanakwambia nini kutokana na siku hii ya UKIMWI



Pia siku hii wanawasha mishumaa

Kunakuwepo pia na maigizo

Mishumaa kwa ajili ya ishara ya amani, upendo na mshikamano kuhusiana na siku hii haikosemani.

Mashairi yenye ujumbe wa siku hii ya kuhamasisha na kuelimisha hayakosekani kutoka kwa watoto wetu wapendwa.

Tuungane pamoja kuwaombea watoto yatima, wajane na pia kuwasaidia pale kwenye uhitaji kwani wanahitaji msaada wako wewe na mimi pia si kwa mali na fedha tu hata kwa maombi yako na kuonyesha upendo wako kwao utabarikiwa na Bwana ukisoma kwenye Mithali 19 :17 Neno la Mungu linasema hivi, "amhurumiaye masikini humkopesha Bwana, naye atamlipa kwa tendo lake jema". Hebu mkopeshe Mungu leo uone jinsi atakavyorudisha deni lake kwa haraka na tena ataweka na faida juu. Zaidi pia Bwana Mungu anasema kuwa yeye ni Baba wa Yatima na mume wa Wajane, unajua kuwa baba hawezi kumwacha mwanae afe kwa njaa lazima atahangaika huku na huko ili awatafutie riziki watoto wake ndivyo hivyo na Mungu wetu alivyo kwa watoto yatima, hebu fanya jambo leo ufanyike kuwa baraka kwa watoto hawa na Mungu atakubariki.