Tuesday, November 16, 2010

NENO LA UZIMA (KUBALI KUJARIBIWA)

Zekaria 13:9

Nami nitalileta fungu lile la tatu na kulipitisha katika moto, nami nitawasafisha kama fedha isafishwavyo, nami nitawajaribu kama dhahabu ijaribiwavyo; WATALIITA JINA LANGU, NAMI NITAWASIKIA; mimi nitasema, WATU hawa ndio wangu; nao watasema BWANA NDIYE MUNGU WETU.

Haya si maneno yangu bali ni maneno ya Bwana Mungu akituambia sisi wana wake wa leo. Mpendwa kubali kupitishwa katika moto kwa maana lipo kusudi la Mungu kufanya hivyo. Ukiona vita vimekuwa vikali ndani ya maisha yako basi usimlau shetani wala usimnung'unikie Mungu kwa kudhania ya kuwa amekuacha ila ujue kuwa Mungu anakupitisha katika moto ili usafishwe kama fedha isafishwavyo utolewa kila aina ya uchafu, visiki hata vile vilivyoweka mizizi yake kwenda chini sana, (kwa maana ya udhaifu wako fulani ambao umekuwa ni vigumu kuuacha ambapo unakupelekea kutenda dhambi) hivi vyote anataka aving'oe ndani ya maisha yako, ili uwe safi. Kisha anakupitisha katika majaribu kwa maana ya kuwa anamwachia shetani akujaribu ili aone kweli umetakata unafaa kuwa chombo chake kiteule.
Majaribu ni mtaji mpendwa wa kukupeleka hatua nyingine katika ufalme wa kiroho, kusudi la Mungu kukupitisha katika moto na pia kuacha ujaribiwe ni kukusafisha na kukufanya uwe safi kama yeye alivyo kwani Mungu wetu hakai mahali palipo pachafu kwa sababu yeye ni Mtakatifu. Na ili wewe uwe Mtakatifu kama yeye alivyo ni kwa kusafishwa ndio maana anasema katika maandiko yake kuwa iweni watakatifu kama mimi nilivyo Mtakatifu. Sasa je wawezaje kuwa Mtakatifu kama bado unao uchafu ndani yako? Na hakuna awezaye kuuona uchafu uliokuwa nao isipokuwa yeye pekee ndiye aonaye hata ndani ya mioyo yetu na yeye ndiye anayeweza kukutoa yale ambayo kwa macho ya  nyama ya kibinadamu hatuwezi kuyaona ambayo yamekuwa changamoto kubwa katika maisha yako na kufanya usiweze kutumiwa na Bwana au yamekuwa kizuizi kikubwa cha wewe kufanikiwa. Kutokuwa msafi pia ndipo kunakopelekea hata maombi yako yanakuwa hayapokelewi kwa maana ukimwita Mungu anakuwa hakusikii maana anasema akishakusafisha na kukujaribu na kukuona safi ndipo utakapomwita jila lake naye atasikia.
Ukisoma katika 1Wakoritho 10:12 utaona ya kuwa Mungu ni mwaminifu hata akiaacha ujaribiwe anafanya pia na mlango wa kutokea katika hilo jaribu. Hivyo basi Mungu haruhusu majaribu yakupate kama hana kusudi jema nawe anachotaka ni wewe kumtumainia na kuamini kuwa anaweza kufanya yasiyowezekana yakawezekana cha msingi ni kuzidi kulitukuza jina lake, kumsifu na kushika maagizo yake na kutenda hasa hasa pale unapokuwa umepitishwa kwenye moto.
Faida ya kukubali kupitishwa kwenye moto na kujaribiwa ni kuwa utakapoita jina lakeanasikia tena kwa haraka sana anasema kuwa hakika utasema Bwana ndiye Mungu wako kwani atakutendea mpaka yale ambayo uliyokuwa hukuyaomba. Atafungua madirisha ya mbinguni na baraka zake zikushukie atakubariki uingiapo na utokapo, atabariki watoto wako, ndoa yako na hata familia yako kwa ujumla. Hata sahau kazi ya mikono yako kwani nayo pia itabarikiwa, atabariki mifugo yako na mazao yako shambani. Ukisoma katika Isaya 65:20-25 utaona ahadi nyingine za baraka kutoka kwa Mungu na ni jinsi gani utakavyoweza kufanikiwa katika maisha yako ukikubali kusafishwa.
Mungu wetu analokusudi jema nawe mpendwa kwani anakuwazia yaliyo mema siku zote. Hivyo basi kubali kupitishwa katika moto usafishwe uwe safi nawe uuone mkono wa Bwana ndani ya maisha yako.

NENO LA MUNGU LIGONGELEZEWE KATIKA VIBAO VYA MIOYO YETU.

No comments: