Monday, November 22, 2010

TUKIWA NA YESU TUNAYAWEZA YOTE

Bwana wetu Yesu Kristo anatuambia hivii,

Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa baba ila kwa njia ya mimi.

Pia Yesu anaendelea kusema hivii,

Amin, amin nawaambieni, Yeye aniaminie mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya, naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa baba. Nanyi mkiomba lolote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili baba atukuzwe ndani ya mwana.

Tutafakari mistari hii je Bwana Yesu alikuwa na maana gani alivyokuwa anasema maneno haya? Je unaamini kuwa bila Yesu hautaweza kuuona ufalme wa Mungu? Basi sasa kama bado haujampokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi ndani ya maisha yako tafakari kwa makini kuhusu mstari huu. Mpokee leo naye atabadili hali ya maisha unayoishi sasa na utapata burudiko la moyo na furaha ya kweli kwani yeye ndiye njia pekee ya wewe kuweza kumwona Bwana.

Je unajua kuwa ukimwamini Yesu na kazi alizozifanya angali hapa duniani na wewe waweza kufanya kama yeye na kubwa kuliko alizozifanya Yesu?  Cha msingi ni wewe tu kumwamini na kuamini kuwa Yesu ni Bwana, na ya kuwa miujiza aliyoitenda na wewe waweza kuifanya. Kwa maana aliyeko ndani yako baada ya kumpokee na kumwamini ana nguvu na ni mkubwa kuliko hayo mapepo, magonjwa nk. Yesu aliweza kumfufua Lazaro aliyekaa kaburini siku nne basi hakika na wewe waweza kufufua. Yesu aliponya vipofu, viziwi na wewe utaweza kuwaponya watu pia anasema na mengine makubwa zaidi yake utaweza kufanya, unachotakiwa ni kumwamini tuuuu.
Anaongeza kusema pia ukiomba lolote kwa jina lake atafanya? haijalishi ni kitu gani unachoomba mradi uombe kwa jina lake Yesu hakika atakutendea, iwe ni amani, furaha, ndoa, watoto, kazi, fedha, na mengineyo mengi atakupa bila hiyana. Tumwamini yeye na tuyashike maagizo yake basi naye atatutendea na pia kwa nguvu ya uweza wake tutafanya mambo makubwa hata yale ambayo kwa akili zetu za kibinadamu yasingewezekana kutendeka na kwa sababu ameahidi na hakika atatenda.

Roho Mtakatifu atuwezesha na atufafanulie kwa hekima yake maneno haya ya Bwana wetu Yesu Kristo na pia yawe ni chachu na nguzo ya kutusogeza karibu na baba na kutuwezesha kuamini.
Barikiwa mpendwa.

No comments: